Friday, May 10, 2013

POLISI WATATU WAKAMATWA NA FUVU LA KICHWA CHA BINADAMU.....WALITAKA KUMPAMBANISHA MTU KESI


Jeshi la Polisi limeendelea kupata kashfa, baada ya askari wake watatu mkoani Morogoro na raia mmoja kushikiliwa kwa tuhuma za kukutwa na fuvu la kichwa cha binadamu ambalo walikuwa wanalitumia kubambikia watu kesi.


Askari hao wanaofanyakazi katika wilaya ya Kilosa wanadaiwa kujaribu kukitumia kichwa hicho kutaka kumbambikia kesi mfanyabiashara mmoja mkoani humo.

Fuvu hilo linadaiwa ni la mtu aliyeuawa hivi karibuni kati ya wilaya za Kilosa na Mvomero mkoani humo.


Tukio hilo limevuta hisia za watu wengi ambao walikusanyika katika kituo cha polisi katika mji wa Dumila ambako watuhumiwa hao wanashikiliwa.

Mmoja wa wananchi hao, Saleh Omar, mkazi wa Dumila, aliwatuhumu askari hao kushirikiana na raia mmoja kumbambikia kesi hiyo mfanyabiashara ya maduka katika mji wa Dumila, Samson Mura.

Alisema Jumatatu wiki hii, walifika askari watatu na raia mmoja ambaye naye alijitambulisha ni askari wakiwa na mfuko usiojulikana ndani yake kuna nini na kwenda nyumbani kwa mfanyabiashara huyo wakitaka kumfanyia upekuzi nyumbani kwake kwa madai kuna vitu vya wizi amevihifadhi.

Hata hivyo, Mura aliwaruhusu askari hao watatu na raia huyo aliyejitambulisha kuwa ni askari kuingia katika nyumba hiyo na kuanza upekuzi, lakini hawakufanikiwa kupata kitu chochote.


Baadaye askari hao walimtaka mfanyabishara kutoka nje na kufungua gari lake ndogo milango ya mbele, lakini nako hawakukuta kitu na baadaye mlango wa nyuma na ndipo walipokiweka kichwa hicho kwa siri na kumtuhumu kuwa alikuwa amefanya mauaji.


Naye Musa Magisa alisema kuwa wakati tukio hilo linatokea kulikuwa na baadhi ya wananchi ambao walishuhudia kitendo hicho na kutokukubaliano nacho na hasa baada ya askari hao kutaka wapewa Sh. milioni 25 ili waachane na kesi hiyo.
 

“Sisi tuliwakatalia askari hao kwa kuwa tuliona wazi kuwa walimbambikia mzigo ule ulikuwa ndani na fuvu la kichwa cha binadamu na tukataka suala hilo lipelekwe katika Kituo cha Polisi cha Dumila,” alisema Magisa.

Kwa upande wake, Mura alisema alifuatwa na askari hao watatu pamoja na mtu mwingine aliyejitambulisha ni askari na kumtaka kumfanyia upekuzi katika nyumba yake na yeye hakuwa na shaka na kuwaruhusu kufanya hivyo.
 

“Sikuwa na shaka, niliwaruhusu kuingia ndani kwa kuwa walijitambulisha kuwa ni maaskari, walingia na hawakukuta kitu chochote, walipotoka nje wakaniambia fungua gari wakaangalia mbele wakakosa baadaye katika milango ya nyuma ndiyo wakadai wamekuta mfuko wenye fuvu la kichwa cha mtu, nikawambia sikuwa na mzigo kama huo kumbe wananchi walikuwa wakifuatilia, waliona walivyoweka,” alisema Mura.

Hata hivyo, alidai kuwa kabla ya kuelekea katika kituo cha polisi, askari hao walimwambia awapatie Sh. milioni 25 ili kumaliza suala hilo, kitu ambacho alikipinga na kuwataka kulifikisha Polisi.
 

Naye Mwenyekiti wa Mtaa wa Mgodeni ambako tukio hilo lilipotekea, Zaituni Kifutu, alisema alifuatwa na askari hao wa kituo cha Dumila ambao anawafahamu na mwingine ambaye hakumfahamu na alipomuhoji alisema ni askari mgeni kutoka wilayani Mvomero.

Kifutu alisema baada ya kufanya upekuzi huo katika nyumba ya mfanyabiashara Mura, hawakukuta kitu ndipo walihamia katika gari lake.
 

Aliongeza kuwa baada ya kuona askari hao wakibishana na mfanyabiashara huyo, yeye na wananchi waliamua kulifikisha suala hilo katika kituo cha Polisi Dumila.

Hata hivyo, Kifutu alisema baada ya mahojiano, askari huyo aliyejitambulisha kutoka wilayani Mvomero alikiri kuwa si askari bali ni raia mkata mkaa na kwamba alipigiwa simu na askari hao kushirikiana naye kumtishia mfanyabiashara huyo ili kujipatia fedha.
 

Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Mkoani Morogoro, Asifiwe Ulime, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo, lakini hakuwa tayari kutaja majina ya askari hao.
 
Hata hivyo, Ulime alieleza kuwa Jeshi la Polisi linawashikilia askari hao pamoja na raia mmoja kwa ajili ya uchunguzi na utakapokamilika, watafikishwa mahakamani.

No comments:

Post a Comment