Thursday, May 2, 2013

NEEMA KWA WALIOFELI FORM 4:..MARKS ZAO ZITAPANGWA UPYA


TUME ya kuchunguza sababu za kufeli kwa kiasi kikubwa kwa wanafunzi wa kidato cha nne waliofanya mitihani ya kuhitimu mwaka 2012 imekamilisha kazi yake na taarifa za uhakika zilizolifia gazeti hili zinasema , upangaji alama zao utafanyika upya.


Kama ambavyo gazeti hili lilivyobaini katika uchunguzi wake wa kiuandishi kwamba kulifanyika mabadiliko ya utoaji alama kwa ajili ya mitihani waliyofanya wanafunzi mwaka huo (2012) bila maandalizi kwa wadau, tume hiyo imependekeza alama zipitiwe upya (regrading).


Katika alama za awali, alama D anapoyopewa mtahiniwa baada ya mtihani wake kusahihishwa ilikuwa ni kuanzia alama 21 kwenda mbele na F ilikuwa 20 kushuka chini lakini katika mabadiliko yaliyoleta ‘maafa’ ya kufeli kwa watahiniwa wa mwaka jana, alama D ilianzia 35 na kuendelea, wakati ile ya kufeli (F) ilianzia alama 34 kushuka chini.


Vyanzo mbalimbali vya habari vimeeleza ya kwamba Jumatatu wiki hii, Baraza la Mawaziri lilikutana mjini Dodoma na kujadili, pamoja na mambo mengine, uamuzi wa kurejea upangaji alama za mitihani hiyo ya wanafunzi iliyosahihiswa kwa kutumia alama za juu (yaani kufeli ni kuanzia alama 34 badala ya 20).


“Baraza limeafikiana na ripoti kwamba upangaji alama ufanyike kwa vigezo vya zamani kwa sababu uamuzi wa kutumia alama mpya ulifanyika bila maandalizi ya kutosha, ikiwa ni pamoja na kutowapa muda wa kutosha wadau.


“Mitihani ya shule na kikanda ilikuwa ikiandaliwa na kusahihishwa kwa alama za zamani, kumbe kulikuwa na alama mpya zimewekwa kitaifa, kwa hiyo kuna uzembe ulifanyika wa kuwafahamisha wadau kwa wakati,” kinaeleza chanzo kimoja cha habari.


Katika uchunguzi wake, Raia Mwema lilibaini kasoro kadhaa zilizochangia kufeli kwa idadi kubwa ya wanafunzi katika mitihani ya kidato cha nne mwaka 2012 na kati ya kasoro hizo ni kutumia alama mpya za kupanga matokeo badala ya alama za zamani, bila kufanyika kwa maandalizi ya kutosha. 


Kutokana na kufeli huko, Februari mwaka huu, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda aliunda tume ili kuchunguza sababu za kufeli kwa wanafunzi wengi waliohitimu kidato cha nne mwaka 2012. Katika matokeo hayo ya kidato cha nne 2012, asilimia 60 ya wanafunzi waliofanya mtihani wa kuhitimu walipata daraja sifuri.


Tume hiyo ilihusisha baadhi ya wadau wakiwamo kutoka shule na vyuo binafsi vya elimu, Kamati ya Bunge ya Huduma za Jamii na Umoja wa Wakuu wa Shule za Sekondari Tanzania (Tahossa), asasi zisizo za kiserikali (NGOs) zinazojishughulisha na masuala ya elimu.

RAIA  MWEMA

No comments:

Post a Comment