Monday, May 20, 2013

"MNAOTAKA URAIS ANZENI KUPITAKUPITA ILI MJULIKANE".....HII NI KAULI YA RAIS KIKWETE



MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Jakaya Kikwete amefungua milango kwa kuwataka baadhi ya watu ndani ya chama hicho wanaowania urais mwaka 2015 kuendelea na mchakato huo.

Rais Kikwete amewatahadharisha watu hao kuendesha kampeni zao kwa ustaarabu pasipo kuibua chuki wala kujenga makundi ambayo alisema ni hatari kwa kuwa yanaweza kukipasua chama. Rais Kikwete aliyasema hayo katika mkutano ndani wa wabunge wa chama hicho uliofanyika jana katika ukumbi wa CCM (white house) mkoani Dodoma.

Mkutano huo ambao ulianza saa 3.00 asubuhi ulilenga kujadili masuala mbalimbali ya taifa ikiwamo utekelezaki wa ilani ya uchaguzi ya chama hicho katika majimbo na ahadi mbalimbali za viongozi wa taifa.

 
Chanzo chetu cha habari kutoka ndani ya ukumbi huo kilieleza kuwa Rais Kikwete aliwataka wanachama wenye nia ya kugombea urais kuwa na tahadhari na watu aliowaita vishoka wa siasa.

Kwa mujibu wa chanzo hicho, Rais Kikwete alisema watu wa aina hiyo wana tabia ya kula huku na huku kwa kujiingiza katika kambi zaidi ya moja.

“Tuangalie makundi ya urais 2015 yasishambuliane kwa kuvunja chama, wenye nia hiyo ya kugombea waendelee na mikakati yao bila kujenga chuki kwa makundi mengine.

“Katika hatua hiyo, pia mkumbuke kuwa katika kambi hizo za urais zinatakiwa kujitizama wao na wafuasi wao maana wafuasi wengine hawaaminiki, ” alisema Rais Kikwete.

Kwa mujibu wa chanzo hicho, miongoni mwa ajenda alizokuwa nazo Rais Kikwete ni pamoja na suala la urais na utendaji wa wabunge majimboni.

Rais Kikwete aliwataka wabunge wa chama hicho kubadili mwenendo wa kuyatelekeza majimbo yao na badala yake akawahimiza kujenga tabia ya kutembelea majimbo yao mara kwa mara.

“Hili JK amelisemea kwa ukali kwamba tabia ya baadhi ya wabunge kuhamia mijini na kutelekeza majimbo yao ni hatari kwani mwisho wa siku wananchi watawanyima kura na kuzipeleka upinzani.
 

Pia alikemea tabia ya baadhi ya wabunge kununa na kuwachukia watu wengine wenye nia ya kugombea katika majimbo yao. Akasema mbunge asiyetimiza wajibu wake kwa wananchi wake na bungeni ni vigumu kubaki.

“Wanatakiwa kurudi majimboni kwao kusimamia ilani ya chama pamoja na ahadi zao walizoahidi na zile za viongozi wa chama na Serikali ikiwamo ahadi zake kama rais,” alisema.

Kuhusu suala la ukosoaji, Rais Kikwete alisema wabunge wa chama hicho wana wajibu wa kuikosoa Serikali yao lakini akaonya aina ya ukosoaji wenye lengo la kuibomoa Serikali.

“Mnatakiwa kuisimamia Serikali na kuikosoa bila kuibomoa, lakini kuna baadhi yenu mmekuwa mkiibomoa Serikali kwa jinsi mnavyochangia huko bungeni… hilo si jambo jema hata kidogo, waachieni wale wenzetu,”alisema Kikwete.

Chanzo hicho kilieleza kuwa wabunge wamekuwa hawaridhishwi na utendaji wa baadhi ya mawaziri ambao walisema ni mizigo na kutaka waondolewe katika nafasi zao.

Chanzo hicho kilitaja majina ya mawaziri hao wanaodaiwa kuwa ni mizigo kuwa ni Waziri wa Mifugo na Maendeleo ya Uvuvi, Dk. David David Mathayo, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa na Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Fenera Mkangara.

Baadhi ya wabunge walimtaka Rais Kikwete kudhibiti ubadhirifu unaofanywa na baadhi ya watendaji wa halmashauri mbalimbali nchini, wakuu wa wilaya na wakuu wa mikoa.

“Rais anatakiwa kukunjua makucha yake kuondokana na uozo huu katika halmashauri zetu. Haiwezekani waendelee kunyamaziwa, tunatakiwa kuimarisha chama kwa kuangalia namna Serikali inavyoweza kutimiza ahadi kwa wananchi,” kilisema.

Kiliendelea kusema. “Serikali iweze kusaidia katika kutimiza ahadi kwa kutelekeza ilani ya chama, viongozi wa vijiji, kata na vitongoji kuanza kulipwa mshahara maana wamejitolea kwa muda mrefu hivyo huwalazimu kupata ushawishi kutokana na njaa,” kilisema.

Imeelezwa kuwa katika kikao hicho kinachoendelea kitakuwa na ajenda nyingi ambazo zitaibuliwa na wabunge.

Hizo ni pamoja na maslahi ya wabunge, utendaji kwa baadi ya mawaziri na aina ya ukosoaji inayofanywa na baadhi ya wabunge wa chama hicho.

Baada ya mapumziko ya mchana, kikao hicho kiliendelea kwa wabunge kupata nafasi ya kujadili hoja mbalimbali kutokana na hotuba ya Rais Kikwete aliyoitoa asubuhi.

Rais Kikwete anakutana na wabunge hao wakati wenyewe wanaonekana kugawanyika kutokana na kuwapo kundi la wabunge wanaoitetea Serikali na wengine wanaoikosoa.

Miongoni mwa wabunge wanaoikosoa Serikali ya chama hicho waziwazi ni Mbunge wa Mwibara, Kangi Lugola, Mbunge wa Ludewa, Deo Filikunjombe, Mbunge wa Kisesa, Luhaga Mpina na Mbunge wa Nkasi Kaskazini, Ally Keissy.

Hata hivyo, chanzo hicho kilieleza kuwa wabunge hao machachari walichanwa hadharani na baadhi ya wabunge wanaoiunga mkono Serikali hali inayoonyesha kuwa wabunge hao si wamoja.

Mbunge wa Sikonge, Said Nkumba alisimama na kueleza kuwa anashangazwa na aina ya ukosoaji unaofanywa na wabunge hao na kusema. “Kama hawataki kufuata maelekezo ya chama wahame,” alisema.


No comments:

Post a Comment